Friday, April 17, 2009

2010 NAHISI WATU WATAKIMBIA TAALUMA ZAO!

Ushindani utakuwa mkubwa

Ndugu wasomaji wa blog hii, kwanza samahani kwa kutoonekana katika kibaraza hiki kwa muda mrefu kidogo. Hii nikutokana na mlundikano wa majukumu niliojiwekea, ambayo naoan kama vile yananielemea. Hata hivyo kwa kuwa maji nimeshayavulia nguo sina budi kuyaoga.

Ndugu wasomaji na wanablog wenzangu ukimya wangu haukuwa ni wa bure, bali pamoja na mambo mengine, lakini nilikuwa najaribu kutafuta changamoto mbalimbali zinazotukabili sisi vijana, ili niweze kuziweka hapa tuweze kujadili kwa pamoja.

Kwa kuanzia, kuna jambo moja ambalo nimekuwa nikijiuliza, naamini labda si mimi peke yangu, lakini inawezekana wapo ambao nao kwa upande wao wanajiuliza kuhusu jambo hili.

Kama inavyojulikana kuwa Mwaka 2010 ni mwaka wa uchaguzi mkuu, uchaguzi ambao utatupa fursa sisi wananchi kumchagua Rais wa nchi hii pamoja na Wabunge,
Swali ninalojiuliza ni hili, kwa kuwa imeonekana kuwa siasa ina tija kuliko kazi nyingine za kitaaluma, kazi kama Uhadhiri, Udaktari, uinjinia uhasibu, uanasheria nakadhalika nakadhalika.
Hii haiashirii kuwa kuna uwezekano mkubwa wa wasomi wetu, hasa vijana kukimbilia siasa kwa wingi na kutelekeza taaluma zao ili kujihakikishia kipato?

Kama inavyojulikana kuwa mishahara ya serikali ni midogo na hivyo kusababisha pensheni nayo kuwa kiduchu, sasa huu si ushahidi tosha kuwa kazi za kitaaluma hazilipi, na badala yake siasa ndio yenye kulipa?

Wote tumemsikia Mheshimiwa Wilbrod Slaa mbunge wa Karatu kupitia CHADEMA, akielezea kuhusu ukwasi unaopatikana pale Bungeni.

Je hii haiashirii kwamba huenda mwakani nchi ikakumbwa na uhaba mkubwa wa wataalamu hawa katika sekta za Elimu, afya, Miundombinu, Sheria, na nyingenezo?

Mimi sio mtabiri, lakini kila nikiangalia kwa makini, naona kama hili huenda likatufika.
Hii nadhani ni changamoto yetu wote kama anavyosema Mzee wa Changamoto kaka Mubelwa Bandio.