Monday, March 30, 2009

UMOJA WA VIJANA KWA MASLAHI YA NANI?

Tuna hitaji tupate chombo cha kusemea

Ndugu wasomaji wa blog hii ya vijana, kuna jambo moja linanitanza, ningependa tutafakari kwa pamoja.
Jambo lenyewe ni kuhusu kitu kinachoitwa Umoja wa Vijana, Tangu kuzaliwa kwangu mpaka kukua kwangu sijawahi kusikia kuhusu umoja wa vijana. Hapa sizungumzii umoja wa vijana wa CCM, Chadema, NCCR Mageuzi au sijui chama gani huko.

Nazungumzia umoja wa vijana unaowaunganisha Vijana wote nchini bila kujali itikadi zao za kivyama, kidini, kikabila au kikanda.
Nimekuwa nikijiuliza, hivi sisi tunao umoja wa vijana unatuunganisha vijana wote hapa nchini? Umoja ambao tunaweza kuutumia kama jukwaa letu sisi vijana kusemea mambo yetu na kujadili mustakabali wa maisha yetu?.

Naomba munisaidie wadau, hivi hapa nchini tunao umoja wa Vijana wa aina ninayoizungumzia? Na kama upo, makao makuu yake yako wapi na unafanya nini kwa sasa?
Kama umoja wa vijana wa aina hii haupo, basi nadhani wakati sasa umefika kwa vijana kuuwasha moto, Lipigwe la mgambo ili vijana wote nchini tuungane katika kutetea maslahi yetu, tumekandamizwa kiasi cha kutosha, na sasa nadhani wakati umefika kwa sisi vijana kusema basi imetosha, wazee wakae pembeni vijana tushike hatamu za uongozi katika nchi hii.

Labda wadau walioko ughaibuni watusadie, kutuelimisha kuwa huko waliko vijana wenzetu wamewezaje kuunganisha nguvu zao, na kuisaidia jamii katika kujiletea maendeleo? Na wamewezaje kushirikishwa katika maamuzi ya kiserikali pale yanapozungumziwa mambo yanayowahusu?

Tumekuwa tukiambiwa kuwa vijana ni taifa la kesho, hee! Ni kesho gani hiyo isiyofika? mimi naamini kuwa kesho hiyo haipo na haitakuwepo mpaka tuende kaburuni. Huu ni wakati wa vijana kuingia kwa wingi katika siasa ili tujiletee ukombozi.

Kuna maamuzi mengi mazito yanayowahusu vijana hapa nchini ambayo yamepitishwa na wazee wetu bila kutushirikisha na sasa tunaumia, kwa mfano mfumo wetu wa elimu umepogoka, na umekuwa na mizengwe.
Kuna mambo mengi ambayo yanatuhusu na yanahitaji umoja huru wa vijana usiofungamana na chama chochote ili tuweze kuyasema.

Naomba kuwasilisha…..

Friday, March 27, 2009

HEBU TUTAFAKARI KWA KINA

Wamepoteza matumaini kabisa

Hivi karibuni nilihudhuria kongamano moja la vijana, ambalo lilikuwa likijadili changamoto zinazowakabili vijana katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na matatizo ya kuyumba kwa uchumi.

Mmojawapo wa waliokuwa wawezeshaji wa kongamano hilo alikuwepo raia mmoja kutoka nchini Marekani. Mwezeshaji huyo alisema kuwa katika kipindi hiki ambacho uchumi umeyumba dunianai waaathirika wakubwa ni vijana, kwani kuna mamilioni ya vijana hapa dunianai wamepoteza ajira na hawajuia hatma yao. Alisema kuwa nchi za ulaya na Marekani anakotoka kuna kundi kubwa la vijana ambao wametupwa nje ya ajira na sasa hivi wana hali mbaya sana kimaisha.

Aliendelea kusema kwamba mfumo wa elimu katika nchi nyingi hauwaandai vijana kujiajiri na badala yake huwaandaa kuajiriwa, na hiyo ndio changamoto wanayopata vijana wengi sana katika kipindi hiki kwa kuwa walisoma wakitegemea zaidi ajira na sasa hivi wanajikuta wakiwa nje ajira na hakuna pa kukimbilia kwani kila mtu amejengwa kiakili kuwa kusoma ni kuajiriwa na ukimwambia ajiajiri unakuwa kama unampa kitendawili kigumu asichoweza kukitegua.

Mwezeshaji huyo alishauri kuwa, kuna haja ya kubadili aina ya ufundishaji mashuleni, pamoja na masomo ya kitaaluma lakini elimu ya ujasiriliamali ipewe kipaumbele zaidi ili kuwawezesha vijana kukabiliana na chanagamoto kama hizi zinapotokea.

Hii naona ni changamoto kwetu sisi vijana, inabidi tuanze kuangalia mustakabali wetu kwa jicho la tatu. Je kuna haja ya kusoma huku tukitegemea ajira au tubadili mtazamo wetu na kuangalaia zaidi namna ya kujiajiri?
Je mfumo wetu wa elimu unakidhi hali halisi tuliyo nayo sasa au ubadilishwe kabisa na kuanzishwa mfumo utakaokidhi matakwa ya hali tuliyo nayo sasa.

Kuna wakati nilisoma mjadala mmoja aliouanzisha dada Koero pale kwenye kibaraza chake cha Vukani, akiuliza “Msomi hasa ni nani?” Sidhani kama swali lile lilijibiwa ipasavyo kwani niliufuatilia sana ule mjadala lakini nikaachwa hewani nisijue niamini nini?
Mitazamo ilikuwa ni mingi na kukinzana kulikuwa kwingi pia, kwa hiyo mwishio wa siku nikaachwa bila jibu.

Naomba tutafakari kwa kina, nini kifanyike ili kukabiliana na changamoto kama hizi za kuyumba kwa uchumi?
Hapa tunatafuta Muarobaini utakaotuvusha hapa tulipo na wakati huo huo tukiweka kinga kwa majanga ya namna hii huko mbeleni

Naomba kuwasilisha

Thursday, March 26, 2009

UTAMBULISHO WA BLOG MPYA

Wasichana ndio wanaopambana na changamoto nyingi tofauti na wavulana

Kama nilivyoeleza hapo juu kuwa blog hii ya Behavefree ni blog itakayokuwa inajadili tabia mbali mbali za vijana ikiwa ni moja ya changamoto zinazowakabili vijana katika kufikia malengo yao ya baadaye katika jamii.

Je kutokana na changamoto hizo wamewezaje kubadili tabia zao na kufikia malengo yao na hatimaye kupata mafanikio katika kuendesha maisha yao?

Blog hii itakuwa ikitafuta majibu ya maswali yote yanayowahusu vijana hapa nchini. Pia kutakuwa na habari za kuchangamsha, kufurahisha na kuelimisha.

Hapa nitakuwa nikiibua mijadala mbalimbali, ambayo itakuwa ikiwasaidia vijana kutafakari upya mustakabali wa maisha yao kutokana changamoto zinazowakabili katika masuala ya elimu, ujasiriamali, siasa, na maisha kwa ujumla.

Natumaini nitapata ushirikano kutoka kwa wanablog wenzangu walionitangulia katika uwanja huu wa blog pamoja na wasomaji kwa ujumla.

Natarajia kupata ushirikianao wenu.